WATUHUMIWA WA MAUAJI JIJINI MWANZA NA TANGA WAUAWA DAR ES SALAAM. - Rhevan Media

WATUHUMIWA WA MAUAJI JIJINI MWANZA NA TANGA WAUAWA DAR ES SALAAM.

MTU mmoja anayedaiwa kuhusika katika mauaji yaliyotokea katika Msikiti wa Rahma, jijini Mwanza ameuawa.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo limeeleza kumuua Salum Saidi Muhangwa (30) kwa madai ya kuwa miongoni mwa waliofanya mauaji kwenye msikiti huo.

Akizungumza na wanahabari Simon Siro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam amesema, mtu huyo ameuawa leo asubuhi wakati akijaribu kuwakimbia polisi kupitia dirishani.

“Baada ya kufanya mauaji kule Mwanza na kikundi chake walikimbilia huku Dar es Salaam, taarifa za raia wema zimetuonesha jambazi huyo alikua anaishi Buguruni,” amesema.

Mauaji hayo yalifanyika tarehe 19 Mei mwaka huu katika msikiti huo uliopo kwenye Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana ambapo watu watatu, waumini wa msikiti huo waliuawa wakati mwingine mmoja  akijeruhiwa.

Kamanda Sirro amesema, mtu huo baada ya kugundua kuwa askari wamezunguka jengo alilokuwemo, alijaribu kujihami kwa kuwarushia askari bomu la mkono ambapo askari walifanikiwa kumpiga risasi ya mguu hatimaye kufariki wakati akipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Tunashukuru askari hawakufanywa lolote katika tukio hilo na tunashukuru kwa sababu wapo makini,”amesema Kamanda Sirro.

Hata hivyo amesema, mtu huyo amefanya matukio mengi pale Mwanza yakiwemo kufanya unyang’anyi katika vituo vya M-Pesa, Tigo Pesa, uchinjaji watu msikitini pamoja na maduka makubwa.

“Kuna timu yake imebaki hapa Dar es Salaam lakini tuwahakikishie wana Dar es Salaam kwamba, tutawakamata na haki itatendeka lakini wakikaa vibaya wasilaumu serikali.

“Kwa sababu silaha wanazozitumia hawajanunua madukani, wanakaa nazo visivyokua halali wabadilike wawe raia wema itawasaidia lakini kwa staili hii niwaambie wataacha familia zao kwa sababu ukamataji wa mtu mwenye silaha sisi ndio tunajua namna ya kukamata,”amesema.

Katika tukio jingine, Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata jambazi sugu aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdallah akiwa na bastora aina ya nolinko, risasi 19 na bomu la kutupa kwa mkono.

“Baada ya kufanya mauaji Tanga na kikundi chake walikimbilia hapa Dar es Salaam, naye akachomoka na kuanza kupambana na polisi, na askari wetu waliweza kumjeruhi vibaya sana naye wakati akipelekwa hospitali alifariki dunia."

Kamanda Siro amesema mtu huyo ni kiongozi mkubwa aliyebaki katika kundi la majambazi mkoani Tanga na amehusika katika mauaji ya watu wanane pamoja na  ujambazi uliofanyika katika kituo cha mafuta mjini humo.

“Wananchi na hasa raia wema waendelee kutupa taarifa kwa watu wanaowatilia mashaka,” amesema.
Previous
Next Post »