Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja na
waheshimiwa wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini
Dodoma.
Watoto wenye ulemavu
wakiwakilishwa na viongozi wa mabaraza ya watoto wenye ulemavu kutoka
mikoa mbalimbali nchini, wamepata nafasi ya kukutana na wabunge ambao ni
wajumbe wa kamati ya Katiba na Sheria na kuanika changamoto zao.
Tukio hilo lilichukua nafasi hivi
karibuni baada ya watoto hao kwa msaada wa Free Pentecostal Church of
Tanzania (FPCT) kupata fursa ya kuhudhuria vikao vya bunge mjini Dodoma
kisha baadaye kufanya mkutano ndani ya Ukumbi wa Pius Msekwa
uliowajumuisha walezi wao, wabunge na mawaziri.
Wakieleza changamoto zao mbele ya
wabunge hao pamoja na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri (Ofisi ya
Waziri Mkuu) Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu , Abdallah
Possi, watoto hao waliweka bayana mambo mbalimbali yanayowapa wakati
mgumu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na jinsi wasivyopata haki sawa
na watoto wengine.
Baadhi
ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja waheshimiwa
wabunge na mawaziri nje ya Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Akisoma risala akiwawakilisha watoto
wenzake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wenye Ulemavu Tanzania,
Wilfred Wilbert alisema kwanza anawashukuru FPCT kwa namna ambavyo
wameweza kuwasaidia kuwaweka pamoja, kutambua na kuzidai haki zao za
msingi.
“Mabaraza ya watoto wenye ulemevu
yametuunganisha na kutupa wakati mzuri wa kujadili pamoja changamoto
zinazotukabili katika mikoa yetu, tumekuwa tukipaza sauti zetu na hata
wakati mwingine kushirikiana na viongozi mbalimbali kuwaanika wale ambao
wamekuwa wakificha watoto walemavu.
“Changamoto tunazopitia zinazokwamisha
malengo yetu ni nyingi lakini nipongeze serikali ambayo kwa namna moja
ama nyingine kupitia sauti zetu wamekuwa wakifanyia kazi mambo kama vile
miundombinu,” alisema mtoto huyo.
Naye Mhazini wa Watoto Wenye Ulemavu
Mkoa wa Tabora, Mpaji Nicolaus alipata nafasi ya kueleza changamoto
zinazowakumba ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kuendeshea vikao
vya mabaraza na kusafirisha watoto kutoka sehemu moja hadi nyingine
pamoja na vifaa vya kutunzia ‘dokyuments’.
“Serikali itenge bajeti maalum kwa ajili
ya pesa za kuendesha mabaraza haya. Lakini pia wadau mbalimbali
wajitokeze kusaidia mabaraza haya. Kompyuta za kutunzia nyaraka
mbalimbali za mabaraza haya ni tatizo pia,” alisema Mpaji.
Naye, Christina Majugwe ambaye ni
Katibu wa Baraza la Watoto Wenye Ulemavu Taifa alizitaja changamoto
nyingine zinazowakabili watoto wenye ulemavu kuwa ni kutotekelezwa kwa
sheria, sera, taratibu na miongozo inayowahusu wao, hali inayopelekea
kujihisi wametengwa.
“Tunawaomba waheshimwa wabunge
mtusaidie katika kuishauri serikali ili hizi sheria zinazotuhusu sisi
ziweze kufanya kazi kuanzia ngazi ya chini hadi juu,” alisema mtoto
huyo.
Akizungumzia changamoto ya fedha kwa
ajili ya kuwasaidia watoto walemavu, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Rashidi
Shangazi alisema kuwa, ni vyema kukawepo fungu maalum kutoka serikalini
la kuwasaidia watoto hao badala ya kutegemea wasamaria wema.
“Tusiwasaidie watoto hawa kwa staili ya
mwenye nacho atoe, kuna suala la kuchoka na kwamba wanaowasaidia
wanaweza kuchoka na watoto hao wakabaki kwenye mazingira magumu. Kuwepo
na mfumo maalum wa kuwawekea mfuko wao wa fedha za kuwasaidia,” alisema
Shangazi.
Mbunge huyo pia akatumia fursa hiyo
kuwapongeza FPCT kwa kazi ya kiroho ya kuwasaidia watoto hao na akamtaka
Waziri Possi kuangalia njia nzuri ya kuwasapoti ili waweze kufikia
malengo yanayotakiwa.
“Hizi jitihaza hazitakiwi kuachwa kwa
kanisa. Mifuko ya hifadhi ya jamii iwaangalie watoto hawa. Naahidi
nitakuwa mbunge maalum wa kuwatetea sehemu yoyote.”
Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel
Mwakasaka alisema kuwa, watoto hao walemavu wanatakiwa kuchukuliwa kama
watoto wengine kwa kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi na kikubwa
elimu iendelee kutolewa ili watu wajue umuhimu wa kuishi nao vizuri.
“Wakati tunaangalia jinsi ya kuwasaidia, nyie wenyewe muwe wamoja, mpendane, msibaguane ili iwe rahisi kwa jamii kuwasaidia.”
Alipopewa nafasi ya kusema chochote, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Eng. Stella
Manyanya kwanza aliwapongeza FPCT kwa kazi kubwa wanayofanya katika
kuwasaidia watoto wenye ulemavu lakini pia akiahidi kuzifanyia kazi
changamoto zote zinazoihusu wizara yake.
“Najua kuna changamoto za kutokuwepo
na vifaa vya kutosha vya kufundishia kwa watoto wenye ulemavu na idadi
ndogo ya wakalimani ila niseme tu kwamba wizara yangu katika bajeti
imetenga fedha kwa ajili ya mitaala ya kuwawezesha walemavu kupata fursa
kulingana na mahitaji yao.
“Pia tutahakikisha vinapatikana
vitabu vitakavyowawezesha watoto kujifunza vizuri. Kwa kifupi changamoto
zote tumezichukua na tutazifanyia kazi,” alisema Waziri Manyanya.
Naye Waziri Possi alipozungumza na
watoto hao alionesha kuwaunga mkono kwa jitihada zao za kutetea haki zao
na akawataka kuendelea hivyo hivyo huku akiahidi kuwaunga mkono katika
kila wanachokifanya.
“Vipaumbele maalum vitakuwepo ili watu
wenye ulemavu waishi vizuri. Niseme tu kwamba serikali itafanya kila
inaloweza kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafanyiwa kazi,”
alisema Possi.
Akiizungumzia ziara hiyo, mratibu wa
mpango wa kuwasaidia watoto wenye ulemevu kutoka FPCT, Lucas Mhenga
alisema watoto waliobahatika kukutana na wabunge walifarijika sana na
walitumia fursa hiyo kueleza changanoto zao wakiamini wao wanayo nafasi
kubwa ya kuwasaidia.
“Ilikuwa ni ziara yenye mafanikio
makubwa, watoto walipata nafasi ya kueleza changamoto zao lakini kile
kitendo cha wabunge kuacha majukumu mengine na kutumia muda wao
kuwasikiliza, kimewapata faraja kubwa.
“Tunaamini yale waliyoyaongea
yatafanyiwa kazi ili watoto hawa ambao kwa muda mrefu jamii imekuwa ni
kama imewatenga waweze kuishi maisha mazuri kama wanavyoishi watoto
wengine,” alisema Mhenga.
Sign up here with your email