SIMBA KUPITIA MSEMAJI WAO HAJI MANARA WAIJIBU YANGA.... - Rhevan Media

SIMBA KUPITIA MSEMAJI WAO HAJI MANARA WAIJIBU YANGA....


Awali ya yote klabu inaendelea kutoa pongezi kwa ndugu zetu Waislaam wanaoendelea kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunaamini Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema kwa ibada hiyo muhimu.

Ndugu wanahabari katika siku za karibuni hususan kuelekea mchezo wa Yanga na klabu kutoka Congo DRC  TP Mazembe Englebert kumekuwa na maneno mengi kutoka klabu ya Yanga yakiishutumu klabu yetu kuhusiana na kutokutoa ruhusa kwa mchezaji Hassan Ramadhani ‘Kessy’ na pia kuhusiana na namna mashabiki watakavyokaa majukwaani siku ya mchezo huo Jumanne ya wiki hii.

Klabu ya Simba kwa maksudi kabisa inapenda kutoa ufafanuzi kuhusiana na mambo hayo mawili yanayoleta sintofahamu miongoni mwa wadau wa mchezo huu murua wa kandanda.

Hakuna barua yoyote ambayo klabu ya Yanga imetuandikia kuhusiana na suala la mchezaji Hassan Ramadhani ‘Kessy’ pia hakuna hata mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi wa vilabu hivi ili kutuomba walau kwa mdomo kama taratibu zinavyotaka.
Ikumbukwe Simba huwa haina tatizo kuruhusu matakwa binafsi ya mchezaji na nyote mnajua utamaduni huo wa klabu yetu.

Kwa wasiofahamu mwaka 1998 klabu ya Simba iliwaazima wachezaji watatu Yanga ili wacheze hatua ya makundi kama hii ya klabu bingwa Afrika wachezaji hao ni Shaban Ramadhani Monja Liseki na Alphonse Modest sasa jiulize kama tuliweza kuwaazima wachezaji vipi tushindwe kumruhusu mchezaji waliyemsaini? Pamoja na maneno yao ya kuudhi Simba ni waungwana wa kutosha na wao wasitumie ukimya wetu kuwapotosha wanachama na washabiki wao eti tumewakatalia kuwajibu barua ya Hassan Ramadhani ‘Kessy’
Msimamo wetu kuhusiana na jambo hili inategemea uungwana wao tu.

Pia Yanga kupitia msemaji wao wamenukuliwa kuwa kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe watakaa kwenye majukwaa yote hata yale ambayo kwa utamaduni wa uwanja wa taifa hukaliwa na mashabiki wa klabu yetu.

Tunafahamu kuwa kauli hii ina nia ya kuchochea vurugu kubwa kwenye mchezo huo na sote tunajua athari ya vurugu michezoni tunawashauri Yanga wasijaribu kuleta mashabiki wao kwenye majukwaa wanayokaa washabiki wa Simba ili kuleta amani siku hyo ya mchezo.matarajio yetu vyombo vinavyohusika vitasimamia kwa ukaribu jambo hilo.

Mwisho ingawa si kwa umuhimu klabu haimzuii yoyote kushangilia timu yoyote siku ya mchezo huo kama zilivyo desturi ya wao Yanga kushangilia klabu yoyote inayocheza na Simba hususan wageni toka nje.kama ilivyokuwa miaka michache nyuma ambapo walishangilia na kuvaa jezi za TP Mazembe.

Waarabu wana msemo wao maarufu “KAMA TUDINI TUDANI” kama ulivyofanya na wewe utafanyiwa hivyohivyo.

Imetolewa na
Haji S Manara
Mkuu wa habari
Simba Sports Club
Previous
Next Post »