Jacqueline Wolper Massawe na mkwe wake, mama Harmonize.
DAR ES SALAAM: Siku chache baada
ya staa wa Wimbo wa Bado, Rajab Abdulhan ‘Harmonize’ kumtambulisha
mchumba’ke, Jacqueline Wolper Massawe nyumbani kwao katika Kijiji cha
Mahuta mkoani Mtwara, siri imevuja kuwa wakati wa zoezi hilo, mama mzazi
wa jamaa huyo, anadaiwa kumtilia shaka mrembo huyo juu ya mwanaye na
kumpa wosia mzito.
Rajab Abdulhan ‘Harmonize’na mama yake mzazi.
Chanzo hicho ambacho kilishuhudia hatua
kwa hatua ya matukio hayo kilitunyetishia kwamba siku hiyo baada ya
kufika Mtwara, Harmonize alikwenda nyumbani kwao na Wolper ambapo baada
ya utambulisho, mzazi huyo alionekana kuwa na shaka kwa Wolper juu ya
usalama wa mwanaye.
“Kiukweli Wolper amekubalika kwa mama
Harmonize ila mzazi huyo alionesha shaka kama kweli Wolper ataweza
kuishi na mwanaye maana alidai mastaa wengi wa kike huwa hawadumu kwenye
uhusiano wa kimapenzi, hivyo alionesha kuwa shaka kama kweli Wolper
atakuwa na nia njema na mwanaye au yupo kwa ajili ya kuchota vijisenti
kisha ammwage kama ambavyo wasanii wengine wamekuwa wakifanyiana,”
kilisema chanzo hicho.
Baada ya kumwagiwa ubuyu huo, Wikienda
lilimsaka Harmonize ili kujua kama kweli mama yake alimkubali Wolper au
alionesha shaka naye kama chanzo chetu kilivyotonya. Msanii huyo
aliliambia gazeti hili kuwa kwa namna moja au nyingine mama yake
alimpokea mpenzi wake huyo kwa moyo mkunjufu japokuwa aliwahusia
kuheshimiana na kuvumiliana kwa kila jambo.
“Mama alimpokea vizuri sana kiasi kwamba
hata mimi nilibaki nikishangaa kwani alimpenda na hata kufikia hatua ya
kututaka tuendelee kuheshimiana kwa kila hali kwani njia pekee ya
kufika mbali ni kuheshimiana na kuvumiliana kwa kila jambo japokuwa
kwenye maisha ya kila siku kukwaruzana hakuepukiki,” alisema Harmonize.
Kwa upande wake Wolper aliliambia gazeti
hili kuwa kwenye maisha hakuna raha kama kuishi kawaida kwa sababu
ukawaida ndiyo ulimfanya kukubalika kwa mama Harmonize.
“Hayo ni maneno ya watu lakini
alifurahia sana staili yangu ya kuishi kawaida maana kama ningekuwa na
tabia ya kujiona staa basi watu wasingeweza kunizoea na kunikubali kama
ilivyokuwa kwa mama mkwe,” alisema Wolper.
Wolper na Harmonize walianza uhusiano wa
kimapenzi hivi karibuni huku wengi wakidhani kuwa ni ‘kiki’ kabla ya
mambo kukolea na sasa uhusiano wao umegeuka habari ya mjini.
Sign up here with your email
