LEO
hii jambo hili likisimuliwa ni kama hadithi! Lakini si hadhithi.
Lilitokea miaka ipatayo 52 iliyopita, wakati wasomaji wengi wa safu hii
walikuwa hawajazaliwa na waliolishuhudia walikuwa ama watoto wadogo au
vijana ambao hivi sasa wengi wao ni wazee wa zaidi ya miaka 60.
Ni uasi wa jeshi la ulinzi la Tanganyika
(wakati huo) likiitwa Tanganyika Rifles ulioanzia Kambi ya Colito
Barracks ambayo leo inaitwa Lugalo, ya jijini Dar es Salaam mnamo
Januari 1964. Walioshuhudia tukio hilo – hususan waliokuwa wakiishi Dar
es Salaam – watakumbuka vurugu kubwa iliyozuka katika jiji hilo ambapo
watu waliuawa na mali zikaporwa na askari wa jeshi hilo hususan sehemu
za Magomeni na katikati ya Jiji la Dar.
Watu wachache sana wanaolifahamu tukio
hilo ambalo hata vyombo vya habari huwa havilitaji sana. Lilitokea miaka
ipatayo mitatu baada ya Tanganyika kupata uhuru Desemba 9, 1961 na siku
nane baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Tukio hilo ambalo lilijaza askari wakiwa
na silaha mbalimbali mitaani lilidaiwa lilikuwa la kuibana serikali
iwaondoe maofisa wazungu jeshini, iwapandishe vyeo askari Waafrika na
iboreshe hali ya maisha jeshini.
Uasi huo uliofanyika pia kwa wakati
mmoja huko Kenya na Uganda, nchi zilizokuwa zikitawaliwa na Uingereza,
kwa nchini ulisambaa katika vikosi vingine vya jeshi mikoani kuwaunga
mkono wenzao wa Dar.
Hivyo, wachambuzi wengine walisema uasi huo ulikuwa na nia ya wanajeshi kuziangusha serikali za nchi hizi.
Wakati wa uasi huo, aliyekuwa Rais wa
Tanganyika, Julius Nyerere na makamu wake, Rashid Kawawa, waliikimbia
ikulu ambacho mashuhuda husema walitoroshwa kutoka ikulu katika teksi
moja wakiwa wamevishwa mabaibui na kwenda kujificha Kigamboni.
Kiongozi aliyebaki mitaani wakati wa
vurugu hizo kubwa zilizochukua muda wa siku zipatazo nne, alikuwa ni
waziri wa ulinzi, Oscar Kambona, ambaye wanajeshi walionekana kumkubali
kuwasiliana naye.
Kwa kifupi, uasi huo ulizimwa na
wanajeshi wa Uingereza baada ya Nyerere kuiomba Uingereza imsaidie. Meli
ya kivita ya Uingereza iliyokuwa ikiitwa HMS Centaur ikiwa Aden,
Somalia, ilifika Dar siku ya nne baadaye ikauzima kirahisi uasi huo.
Helikopta kadhaa zilizokuwa katika meli
hiyo ziliibuka juu zikiwa zimening’iniza magari ya Land Rover na kwenda
kutua kambi ya Lugalo yakifuatiwa na askari ambao waliivamia kambi hiyo
na kuwasambaratisha kirahisi askari waasi.
Askari hao walikimbilia mitaani na
vichakani wakitupa silaha na magwanda yao, waliobaki walikamatwa. Huo
ndiyo ukawa mwisho wa uasi huo, na askari wa Uingereza wakachukua nafasi
yao kwani jeshi hilo la Tanganyika Rifles lilivunjwa baada ya Nyerere
kutoka mafichoni.
Baada ya muda, Nyerere aliomba msaada wa
askari kutoka Nigeria ambao walikuja kuchukua nafasi ya askari
waliofukuzwa. Askari hao wa Nigeria walisambazwa sehemu mbalimbali
nchini.
Kwa “vijana wa zamani” waliokuwa Shinyanga, watakumbuka kuwaona askari hao waliokuwa wameweka kambi huko Old Shinyanga!
***Mwisho***
Sign up here with your email
