Beatrice Kiriho enzi za uhai wake.
Richard Bukos na Issa Mnally, UWAZI
Dar es Salaam: Jeshi la Polisi
nchini linamshikilia Fidelis Buberwa, mkazi wa Tabata jijini hapa kwa
tuhuma za kumshushia kipigo mkewe, Beatrice Kiriho na kumsababishia
kifo.
Fidelis Buberwa ambaye ni mume wa marehemu.
Bubelwa anadaiwa kumjeruhi kwa kipigo
mkewe nyumbani kwake, usiku wa Juni 11, mwaka huu kilichomuacha mwanamke
huyo akiwa mahututi na baadaye kukimbizwa Hospitali ya Mwananyamala
kupatiwa matibabu.
Akiwa
hospitalini hapo, Beatrice alitibiwa kwa wiki mbili mfululizo lakini
hakupata nafuu yoyote, Juni 20, mwaka huu akaaga dunia kwa mateso
makali.
Akizungumza
na Uwazi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Beatrice iliyofanyika
Kanisa Katoliki la Tabata Segerea jijini hapa, kaka wa marehemu ambaye
aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema wanandoa hao kabla ya
tukio hilo walikuwa na migogoro ya mara kwa mara ya mapenzi iliyokuwa
ikisababishwa na wivu.
Kaka
huyo aliendelea kueleza kuwa migogoro hiyo ilikuwa ikisababisha wawili
hao kupigana mara kwa mara lakini walikuwa wakisuluhishwa.
Akielezea siku ya kipigo hicho kilichosababisha kifo hicho, kaka huyo alisema:
“Juni
11, mwaka huu, Beatrice alikwenda kwenye harusi ya mtayarishaji wa
muziki aitwaye Manecky (Emmanuel Sewando) ambaye alikuwa akifunga ndoa
siku hiyo, sasa aliporudi mumewe akaanza kumfokea kwa nini alichelewa
kurudi.
“Dada
alimuelezea sababu zilizomchelewesha lakini shemeji inaonekana
hakumuelewa hivyo akaanza kumshushia kipigo mpaka akawa mahututi.
Kufuatia hali hiyo, wasamaria wema walimkimbiza hospitali kupatiwa
matibabu mpaka umauti ulipomfika.
“Ukweli
kifo cha dada yetu kinatupa uchungu sana, inaonesha ni kama vile alijua
hawezi kupona maana akiwa hospitalini mara kwa mara alikuwa
akitusisitiza tumuangalizie watoto wake watatu, ambao wa kwanza ana umri
miaka minne na wengine wawili mapacha wana umri wa mwaka mmoja na miezi
kadhaa,” alimaliza kusema kaka huyo.
Naye
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi, Salum
Hamduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa Beatrice
alifikishwa Kituo cha Stakishari kama majeruhi na kupewa hati namba tatu
(PF3) ya polisi kwa ajili ya kwenda kutibiwa ambapo ndugu zake
walimpeleka Hospitali ya Mwananyamala ambapo alitibiwa mpaka alipopatwa
na umauti.
“Mume
wa marehemu naye alifikishwa kituoni hapo na kufunguliwa jalada la
kujeruhi lakini baada ya kifo hicho jalada hilo limebadilika na kuwa la
mauaji na anashikiliwa na polisi,” alisema Kamanda Hamduni.
Marehemu alizikwa Ijumaa iliyopita kwenye Makaburi ya Tabata Kinyerezi jijini Dar.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amina.
Sign up here with your email