CHADEMA WATAFAKARI HATUA ZA KUCHUKUA BAADA YA RAIS MAGUFULI KUTAKA SIASA ZIFANYWE 2020. - Rhevan Media

CHADEMA WATAFAKARI HATUA ZA KUCHUKUA BAADA YA RAIS MAGUFULI KUTAKA SIASA ZIFANYWE 2020.



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani kimesema kinatafakari hatua gani ya kuchukua baada ya Rais John Magufuli kutaka siasa za nguvu zifanywe wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao, kauli inayotafsiriwa kuwa ni kupiga marufuku shughuli za kisiasa. 

Rais alitoa kauli hiyo mapema wiki iliyopita wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuisisitizia juzi wakati wa hafla ya kuzindua mpango wa polisi wa kuboresha huduma za usalama wa jamii. 

Akizungumza jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, katibu wa Chadema wa kanda hiyo, Casmir Mabina alisema wamefikia azimio la kupinga unyanyasaji na ukandamizaji kwa vyama vya siasa unaofanywa na Serikali ya Dk Magufuli. 

Mabina alisema Rais Magufuli anavunja Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ambayo inaviruhusu vyama vya siasa kuendesha shughuli mbalimbali za kisiasa. 

Alisema vyama haviwezi kukaa kimya mpaka mwaka 2020 wakati kazi yao ni kukutana na wananchi. 
“Tunamshauri Rais Magufuli aache kutawala nchi kwa woga na ubabe ... afuate misingi ya Katiba na sheria, na kuwaongoza Watanzania badala ya kuwatawala,” alisema Mabina. 
 
Mabina aliongeza kuwa Jeshi la Polisi liache kutumiwa na Serikali kufinyanga sheria za nchi na kukandamiza upinzani kwa kutumia vibaya Sheria ya Jeshi la Polisi, kifungu cha 43 (3) kwa kusingizia habari za ‘kiintelijensia’ na ‘hali ya uvunjifu wa amani’. 

Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Dar es Salaam Kuu, Mwita Waitara alilalamikia kitendo cha mameya wa Dar es Salaam kunyimwa vibali vya kwenda nje ya nchi kutafuta fedha ili kusaidia maendeleo ya halmashauri zao. 

Alisema fedha za safari hizo zinatolewa na washirika wa maendeleo, lakini Serikali imekuwa ikizuia safari hizo kwa kisingizio cha kubana matumizi. 

Alisema safari nyingine za nje ni muhimu kwa sababu zinawawezesha mameya kukutana na wadau wa maendeleo ili kupata misaada. 

 “Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alikuwa na safari ya kwenda Afrika Kusini kukutana na mameya wengine duniani, lakini alizuiliwa kwa maelekezo. 

"Hatuwezi kuendelea kama tutashindwa kukaa na wenzetu ili kujifunza mambo ya maendeleo,” alisema.
Mwita alidai kuwa huo ni mpango wa Serikali kudhoofidha halmashauri zinazoongozwa na upinzani ili wasiweze kufanya mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanywa na CCM. 

Alisema yeye pia alizuiliwa kwenda Marekani akiwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii. 
Ushauri mwingine ulitolewa na mwenyekiti wa Kanda ya Ilala, Dk Makongoro Mahanga ambaye alimtaka Rais kufuata Katiba kwa sababu aliapa kuilinda na kuitetea kwa masilahi ya Taifa. 

Dk Mahanga alimtaka Rais akumbuke ahadi mbili alizozitoa wakati wa kampeni na wakati anaapishwa, ambazo ni kuilinda Katiba na kuwaletea wananchi maendeleo. 

“Kinachowaogopesha CCM ni upinzani kupata kura zaidi ya milioni sita wakati wa uchaguzi. Wanajua kwamba wanaweza kuchukua nchi, ndiyo maana wameanza kudhibiti vyama vya siasa ili visiwe na nguvu,” alisema Dk Makongoro ambaye aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Previous
Next Post »