CAG : WAKAGUZI WANGU HAWAHONGWI. - Rhevan Media

CAG : WAKAGUZI WANGU HAWAHONGWI.


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema wakaguzi wake hawayumbishwi au kupewa hongo ili wasihoji zaidi wakati wa kutekeleza majukumu yao japo kuna changamoto zinazoikabili ofisi hiyo, lakini zinaendelea kufanyiwa kazi.
Pamoja na hayo alisema utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kutumia majengo ya serikali katika shughuli zote za semina, warsha na kongamano na mikutano ni zuri kwa kuwa linapunguza gharama kwa serikali tofauti na zilipokuwa zikifanyika katika hoteli ambapo serikali ilikuwa ikitumia fedha nyingi.
Alisema hayo jana katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkaguzi Mkuu wa nje mkoa wa Dodoma kutoka ofisi ya CAG, Martin Madelo wakati wa ufunguzi wa warsha ya usambazaji na ukusanyaji wa maoni ya toleo maalumu ya ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2014 kwa asasi za kiraia na zisizo za kiserikali mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa CAG wakati wa usambazaji wa ripoti, wananchi waliulizwa baadhi ya maswali katika mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa ambao walitaka kufahamu kama wakaguzi hawayumbishwi au kupewa hongo ili wasihoji zaidi.
“Nataka kuwahakikishia kuwa wakaguzi wetu wako makini na wanafanyakazi zao kulingana na maadili ya utumishi wa umma na maadili ya taaluma ya ukaguzi, japo kuna changamoto zinazoikabili ofisi, lakini zinaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.
Alisema pia wadau wamekuwa wakiuliza kama ofisi ya CAG ina uhuru wakati wa kutekeleza majukumu yao na ofisi yake ina uhuru wa kufanyakazi zake na inafuata sheria na taratibu za kazi, hilo husaidia kukamilisha shughuli zote za kiukaguzi kwa wakati.
Alisema wataendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na wamepiga hatua kubwa kufanikiwa kuwapatia wananchi taarifa kupitia toleo maalumu, ingawa bado ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo bajeti ndogo ya usambazaji wa toleo hilo. Pamoja na hayo alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kuhoji serikali yao jambo ambalo limesaidia katika utendaji kazi.
Previous
Next Post »