Seneta wa Vermont Bernie Sanders amemshinda Hillary Clinton katika uchaguzi wa mchujo wa chama cha Democratic katika jimbo la West Virginia, kwa mujibu wa makadirio ya vyombo vya habari Marekani.
Hata hivyo, bado angali nyuma ya Bi Clinton kwa idadi ya wajumbe kwenye kinyang’anyiro cha kumteua mgombea urais wa chama hicho.
Ushindi huo hata hivyo unampa matumaini ya kuendelea na kampeni.
Katika chama Republican, Donald Trump alitangazwa mshindi West Virginia na Nebraska.
Wapinzani wake waliokuwa wamesalia walijitoa kwenye kinyang’anyiro wiki iliyopita.
Lakini mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York anakabiliwa na kibarua kigumu kuwashawishi vigogo wa chama cha Republican kumuunga mkono.
Spika wa Bunge Paul Ryan, afisa wa cheo cha juu zaidi wa kuchaguliwa katika chama hicho, tayari amesema hayuko tayari kumuunga mkono Bw Trump kwa sababu hana msimamo wa kihafidhina.
Ushindi wa Bw Sanders West Virginia, jimbo ambalo Bi Clinton alimshinda pakubwa Barack Obama mwaka 2008, utaendeleza kinyang’anyiro katika chama cha Democratic.
Kwenye hotuba aliyoitoa Salem, Oregon, jimbo ambalo litafanya mchujo wake wiki ijayo, Bw Sanders alishangiliwa sana alipotangaza habari za ushindi wake.
"Sasa tumeshinda mchujo katika majimbo 19 na nataka ieleweke wazi kwamba tumo kwenye mbio hizi kushinda uteuzi wa Democratic."
Pia aliangazia baadhi ya ahadi zake kuu uchaguzini zikiwemo kuondoa ada za mafunzo katika vyuo na kuongeza kodi inayotozwa matajiri.
Pia aligusia hali kwamba kura za maoni zinaonyesha ndiye mgombea Democratic aliye katika nafasi nzuri zaidi ya kumshinda Donald Trump.
Sign up here with your email