Waganga
wafawidhi wa Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wamesema
Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) ni “jipu” linalohitaji kutumbuliwa
kutokana na kuwa na mfumo usioridhisha wa utoaji huduma za dawa.
Wakizungumza
na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, madaktari hao walisema MSD
inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ya utendaji kazi wake, kama siyo
kutumbuliwa kutokana na kuwafanya wafanye kazi katika mazingira magumu
na yasiyo na dawa.
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Azizi Msuya
alisema changamoto iliyopo ni upatikanaji wa dawa na mara nyingi
wanachoomba MSD sicho wanachopata na kinawaletea uhasama na chuki kwa
wagonjwa.
“Wao wananunua palepale na sisi tungeruhusiwa
tungenunua. Maduka kama Salama, kopo moja la dawa aina ya paracetamol ni
Sh7,000, lakini tukinunua kwao inakuwa Sh15,000 la sivyo turuhusiwe
kununua wenyewe kuliko kusubiri dawa mwezi mzima,” alisema Msuya.
Alisema
unaweza kuomba dawa aina nyingi zikiwamo za kuponya maisha haraka kama
za kuzuia damu kutoka, kuzuia kifua kubana, ukapata nyingine hizo
ukakosa. Hivyo kuna hatari ya kufiwa na mgonjwa mkononi.
Dk
Emmanuel Kombe, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makongo alisema
Serikali inapeleka fedha na vituo vina fedha yake, lakini cha kushangaza
utata wa kupatikana mahitaji yaliyoagizwa kila siku upo palepale.
“Wauguzi
wanatukanwa, wanakuwa maadui wa wananchi kwa sababu hospitali hazina
dawa, hakuna mwananchi anayefahamu kama MSD ndiyo hawajaleta,” alisema
Kombe.
Dk Sebastian Mapunda Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya
Kigogo alisema hiyo ni changamoto ya muda mrefu na wao kama watendaji
wanaoshughulika na wagonjwa inawapa shida.
Alisema wananchi
wanapoona dawa katika maduka binafsi halafu hospitali hakuna, wanaona
kama kuna mchezo unafanywa, kumbe MSD wapo kati kukwamisha.
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema atamwandikia barua Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amuombe Rais atumbue jipu la MSD.
Tangu aapishwe kuwa Mkuu wa Wilaya, hiyo ndiyo taasisi ya kwanza kukutana nayo na kusikiliza kero zao.
Alisema
ameanza na afya kwa sababu ndiyo sekta yenye changamoto nyingi ikiwamo
hiyo ya dawa. Hivyo atalishughulikia suala hilo kwa kila njia ikiwamo
kumshirikisha Mkuu wa Mkoa.
“Haiwezekani fedha ipo dawa hakuna
na hakuna jibu la msingi, na haiwezekani dawa kusubiri taratibu mwezi
mzima, wiki tatu kama hakuna ielezwe hakuna ili ufanyike utaratibu wa
kununua zinakopatikana kwa sababu afya za binadamu hazitambui Sheria za
Ununuzi,” alisema Hapi.
Ofisa Habari wa (MSD), Eti
Kusiluka alipingana na madai hayo akieleza kuwa hakuna utaratibu wa
kupokea fedha wanapoagiza dawa zaidi ya kupokea mahitaji ya wateja wao
na kuyafanyia kazi.
“Serikali ina mipango ya ununuzi na muombaji
hupata mahitaji aliyoomba ndani ya siku 14 na 45 na siyo kweli kuwa
fedha zao zinang’ang’aniwa,” alisema Kusiluka.
Sign up here with your email