AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUMUUA MFANYABIASHARA , - Rhevan Media

AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUMUUA MFANYABIASHARA ,


Mahakama Kuu ya kanda ya Dodoma inayoendelea na vikao vyake mjini hapa, imemhukumu mkazi wa kijiji cha Makanda Mpendoo Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida, Adriani Francis Januari (25), adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Adrian amehukumiwa adhabu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuawa mfanyabiashara wa zao la ufuta mkazi wa Nzuguni Dodoma mjini, Enock Kasimba nakisha  kumnyang’anya shilingi 450,000/=.
Aidha, mahakama hiyo iliwaachilia huru washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 52/2014, Rehema Alli (25) mkazi wa Mbagala Dar -es -salaam na Aidani Trancis (14) mkazi wa kijiji cha Makanda Mpendoo wilayani Manyoni. 
Washitakiwa hao waliachiliwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kuwaunganisha na mauaji hayo.
Kaka yake na mshitakiwa Adriani, ambaye anatuhumiwa kushiriki katika mauaji hayo Raymond Francis, aliweza kutoroka na kukimbilia kusiko julikana.
Awali mwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali Petrida Muta, alidai mbele ya jaji Hamisi Hamisi Kalombola kuwa mnamo mei 27 mwaka 2013 muda usiojulikana, mshitakiwa na ndugu zake wengine watatu, kwa makusudi walimuuwa Enock Kasimba kwa lengo la kumpora  Shilingi 450,000.
Muta alisema siku ya tukio Adriani na wenzake walimtuma Aidan kumuita mfanyabiashara Enock kwa madai wanaufuta wa kumuuzia.
Alisema Enock alipofika nyumbani kwa washitakiwa, alikamatwa kwa nguvu na kisha kukabwa koo kwa lengo la kumzuia asipate pumzi, kitendo kilichosababisha kufariki dunia papo hapo.
Mwanasheria Muta, alisema baada ya mfanyabiashara Enock kufariki dunia,washitakiwa hao walibeba mwili wake na kuupeleka hadi mto Bubu wa kijiji hicho cha Makanda Mpendoo.
Akifafanua, alisema washitakiwa Rehema na hasa Aidan ambaye ni mdogo wake na Adriani, ushahidi wao umesaidia kwa kiasi kikubwa  Jamhuri kumtia hatiani mshitakiwa wa kwanza Adriani.
“Aidan ameieleza mahakama jinsi alivyoitumwa na kaka zake kumwita mfanyabiashara Enock na pia alisaidia kuwaonywesha askari polisi kaburi alikozikwa Enock. Mwili wa Enock ulikaa kaburini kwa siku tano ndipo ukafukuliwa kwa ajili ya daktari kuufanyia uchuguzi,” alisema Muta.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Muta, aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotarajia kuuwa binadamu wenzao kwa kukusudia.
Kwa upande wake wakili wa kujitegemea kutoka Dodoma, Simioni Mwigulu aliyekuwa anamtetea Adriani, alisema wanaiachia mahakama kuu, ifanye maamuzi yake.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Hamisa alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umethibitisha bila kuacha chebe chembe yo yote ya shaka na hivyo,mshitakiwa ana hatia ya kosa aliloshitakiwa nalo.
Previous
Next Post »