Mkuu wa Mkoa wa Mara Magesa Mulongo ameagiza maafisa usalama mkoani Mara kufanya uchunguzi mara moja juu ya tuhuma za wauguzi katika zahanati ya Suburu Mkoani humo kufunga zahanati na kusababisha wanawake wawili kujifungulia nje ya zahanati.
Mulongo ameyasema hayo msafara wake ulipozuiliwa na wanakijiji wa Suburu wakimtaka Mkuu wa Mkoa kutatua kero ya wananchi hao ya kukosa huduma stahiki za afya pamoja na kinamama wawili kujifungulia nje wakati Zahanati ipo kijijini hapo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Mulongo amemtaka Daktari wa Zahanati hiyo Dkt. Julius kujibu tuhuma hizo ambapo amekubali na kusema kuwa ni kweli kwa sababu zahanati hiyo haina makazi ya watumishi hao jambo linalofanya usiku kutokuwa na wahudumu.
Aidha Mulongo amesema kuwa pamoja na kutokuwepo kwa makazi ya madaktari katika zahanati hiyo siyo vyema wahudumu wote kuondoka nyumbani kwa kisingizio cha makazi wakati wananchi wanapata shida.
Mkuu huyo wa Mkoa yupo katika ziara ya kuangalia shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi katika wilaya zote 7 za mkoa wa Mara.
Sign up here with your email