WANAHABARI WANATAKIWA KUANDIKA RIPOTI YA ( CAG ) KWA KINA. - Rhevan Media

WANAHABARI WANATAKIWA KUANDIKA RIPOTI YA ( CAG ) KWA KINA.







WAANDISHI wa habari nchini, wamepewa changamoto ya kuandika kwa kina habari zinazotokana na ripoti mbalimbali zinazotolewa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili kuwatendea haki Watanzania.
Changamoto hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, ambaye kwa sasa amestaafu. Kwa mujibu wa Utouh, ripoti hizo zimekuwa zikiripotiwa juu juu, hivyo kufanya mambo mengine yaliyoibuliwa na kuchambuliwa kutofahamika vyema kwa wananchi.
Aidha, alisema, vyombo vya habari nchini vimekuwa vikielezea ripoti hizo kwa kina siku tu zinapotolewa, kuachana nazo baada ya muda mfupi na kuendelea kuutaarifu umma kuhusu mambo mengine.
“Mfano halisi ni ripoti ya CAG iliyotolewa juzi, wanahabari waliziandika kwa kina siku ya kwanza na ya pili tu na kuendelea kuandika mambo mengine,”Utouh alisema na kusisitiza kuwa zinaandikwa bila kuchimbwa vizuri.
Kwa maelezo yake, kwa kutoa ripoti hizo, Ofisi ya CAG inakuwa imetekeleza wajibu wake, hivyo mamlaka nyingine, vikiwemo vyombo vya habari navyo vinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuuelimisha umma kuhusu kazi inayofanywa na Serikali yao,”Utouh alisema na kuongeza kuwa, vinginevyo, inakuwa si kuwatendea wananchi haki.
Aliongeza kuwa ripoti za CAG zinagusa maeneo yote ya utendaji wa kazi serikalini. “Hizi ripoti ni tajiri, nawasihi waandishi wa habari waendelee kujikita kuzisoma na kuwapasha wananchi mambo yaliyoko kwenye ripoti hizo kwa kina,” Utouh alisema.
Katika hatua nyingine, Utouh alimpongeza na kumshukuru Rais John Magufuli kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za CAG, hivyo kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wahusika wanaoguswa kwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kwenye ubadhirifu wa fedha na mali za umma pamoja na waliochangia kuikosesha Serikali mapato.
Utouh aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa kuandaa ripoti hizo ambazo matokeo yake yanaonekana katika utumbuaji wa majipu unaoendelea kufanywa na Rais Magufuli, alisema miongoni mwa hatua hizo ni kutenguliwa kwa uteuzi wa baadhi ya wakurugenzi wa taasisi za Serikali, pamoja na kusimamishwa kazi kwa baadhi yao, kupisha uchunguzi.
Juzi Rais alitangaza kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Ally Simba kwa kushindwa kusimamia mfumo wa TTMS unaoangalia mapato yanayotokana na kampuni za simu.
Ripoti ya CAG kuhusu TCRA ndio iliyoelezea udhaifu huo baada ya kuonesha kuwa hapakuwa na mfumo unaounganisha TCRA na Mamlaka ya Mapato (TRA), hivyo kuwa na uwezekano wa kuinyima mapato Serikali.
Previous
Next Post »