
Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeiagiza serikali kuwachukulia hatua kali wale wote waliovamia miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na kuigeuza kuwa masoko ya bidhaa zao.Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza amesema hali hiyo haivumiliki na inapaswa kukomeshwa mara moja. Kamati hiyo ilikutana kwa mara ya pili na uongozi wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jana jijini Dar es Salaam.“Tumejionea katika ziara yetu tuliyoifanya katika miundombinu ya mradi kuwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wameivamia miundombinu na kuigeuza kuwa masoko,” alisema.Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini alisema jambo hilo haliwezi kufumbiwa macho kwani mradi huo umegharimu fedha nyingi na zitalipwa na kodi ya Watanzania.Alisema pia baadhi ya madereva wa magari na pikipiki maarufu kama bodaboda wameharibu baadhi ya miundombinu na kwamba wanatakiwa kudhibitiwa.Aliitaka serikali kuweka ulinzi na wote wanaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.Aliutaka uongozi wa DART kuipatia majibu kamati yake kulingana na maswali waliyouliza ifikapo Aprili 4 mwaka huu.
Kamati ilitaka kujua miongoni mwa mambo mengine suala la nauli za mabasi, tarehe ya kuanza kwa mradi, na mkataba kati ya DART na mtoa huduma wa mpito wa mradi.
Sign up here with your email