Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Kodi toka Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Bi.Rehema Kilonzi akitoa taarifa kwa waandishi
wa habari kuhusu mapato yaliyokusanywa kutokana na kodi ya pango la
ardhi kwa mwaka fedha 2015/2016 ambapo Serikali imekusanya zaidi ya
Bilioni 60 kati ya bilioni 70 zilizopangwa.kulia kwake ni mwanasheria toka
Wizara hiyo Bw.Seif Hiza na mwisho ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini wa Wizara hiyo Bi Mboza Lwandiko.
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali imesema itawachukulia hatua kali za kisheria wananchi
waliobadili matumizi ya Ardhi ya makazi na kuyageuza kuwa maeneo ya
biashara na kuisababishia Serikali kukosa mapato ya kodi ya Ardhi.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo
Cha Kodi toka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Bi.Rehema Kilonzi wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu
mapato yaliyokusanywa kutokana na kodi ya pango la ardhi kwa mwaka
fedha 2015/2016.
Amesema kuwa baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini
wameyageuza maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya makazi ya watu kuwa
nyumba za kulala wageni,hosteli, maeneo ya biashara kinyume cha Sheria
ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 chini ya fungu la 33.
“Rai yetu kwa wananchi waliopata fursa ya kumiliki maeneo yaliyopangwa
na kumilikishwa kisheria,tunawaomba walipe kodi ya Pango la ardhi kwa
wakati kuepuka usumbufu wa kufikishwa Mahakamani .”alisisitiza Kilonzi.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa 2015/2016 Serikali imefanikiwa
kukusanya kiasi cha Bilioni 60 kutokana na kodi ya Pango la Ardhi ambazo
ni sawa na asilimia 85 ya lengo lililowekwa la kukusanya shilingi bilioni
70.
Amesema mkakati wa wizara hiyo ni kuhakikisha kuwa inafikia lengo la
kukusanya Kodi hiyo na kuongeza kuwa hiyo imesambaza maafisa wake
katika Ofisi zote za Kanda ili kuhakikisha kuwa Halmashauri na Manispaa
zinasambaza hati za madai ya Kodi ya pango la Ardhi na kuwafikia
wadaiwa wote kwa wakati muafaka.
Amesema wizara hiyo inaendelea na mkakati wa kufungua mashauri ili
kupata kibali cha mahakama cha kukamata mali za wadaiwa sugu na
kuwapokonya hati milki katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia hatua hiyo amesema kuwa katika jiji la Dar es salaam
mashauri yataanza kusikilizwa katika Baraza ya Nyumba na Ardhi La
Wilaya ya Kinondoni kuanzia mwezi Mei 2016, kisha zoezi hilo litaendelea
kwa Mikoa na Wilaya zote Jijini hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Kodi ya Ardhi inayotozwa na wizara hiyo
amesema kuwa inatozwa kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Namba 4 ya
mwaka 1999 chini ya fungu la 33.
Amesema kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu ( kuanzia
Februari 2016) Wizara imewafikia wamiliki wa Ardhi 679 katika Maeneo
ya Sinza na Kijitonyama Jijini Dar es salaam na kufanya uthamini wa
maendelezo kwa kwa wale waliokiuka masharti ya matumizi yaliyopangwa
ambapo ilibainika kuwa kuna ukiukwaji wa masharti ya Uendelezaji kwa
kubadili matumizi yaliyoainishwa katika milki zao.
Aidha, amesema kutokana na uthamini uliofanyika mwezi Februari
Serikali inatarajia kukusanya jumla ya milioni mia nane kama faini
kutokana na ubadilishaji wa matumizi ya maeneo usiozingatia Sheria za
Ardhi katika maeneo ya Sinza na Kijitonyama.
Sign up here with your email
