WAKUFUNZI 53 WA JKT WAFUZU MAFUNZO NA KUTUNUKIWA VYETI. - Rhevan Media

WAKUFUNZI 53 WA JKT WAFUZU MAFUNZO NA KUTUNUKIWA VYETI.


WAKUFUNZI 53 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamehitimu mafunzo ya ujasiriamali na kutunukiwa vyeti.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa siku 12 na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Mafunzo hayo yalifanyika katika kambi ya Mgulani na kuhusisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Pwani.
Akikabidhi vyeti hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema wakufunzi hao wana wajibu wa kuwafundisha somo la ujasirimali vijana wanaojiunga na jeshi hilo ili kupambana na tatizo la ajira nchini.
“Mafunzo mliyopata yalilenga kuwawezesha mkawafundishe vijana ili baada ya hapo wajiajiri au kuajiri wengine,” alisema Waziri Mhagama.
Alifafanua kuwa kuwafundisha somo la ujasiriamali, itasaidia kwenda sambamba na soko la ajira katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, utalii, hoteli na kwamba nguvu kazi kubwa ya vijana itakuwa inafanya kazi badala ya kukaa tu na kupenda starehe.
Alisema serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kuwezesha wananchi na jeshi hilo lina nafasi kubwa ya kutumia fursa iliyonayo kusaidia kukuza vijana ili kwa pamoja kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.
Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Michael Isamuhayo, alisema jeshi hilo limejipanga kuwafundisha vijana wanaopitia mafunzo hayo ipasavyo ili wawe chachu ya kukuza vipato vyao na uchumi wa nchi.
Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema utoaji wa mafunzo hayo kwa wakufunzi wa vijana kwa jeshi hilo ni utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Aliwahimiza vijana wanaohitimu masomo wajiunge na mafunzo ya JKT kwa wingi na huko watakutana na mafunzo hayo yanayolenga kuwajenga kujitegemea.
Kwa mujibu wa program hiyo, kanda itakayofuata itakuwa ya Kati na Magharibi itakayojumuisha mikoa ya Dodoma, Kigoma, Tabora na Mwanza,”alisema.
Mafunzo yatafanyika katika kambi ya Makutopora, Dodoma.
Mafunzo katika kanda ya Kusini yatafanyika Mafinga ikihusisha mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa na Njombe.
Mafunzo kwa Kanda ya Kaskazini yatafanyika katika kambi ya Mgambo mkoani Tanga na kuhusisha mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.
Tangu kurejeshwa kwa utaratibu wa mafunzo ya vijana wa kujitolea mwaka 2001 idadi ya vijana wanaojiunga na JKT imeendelea kuongezeka kila mwaka.
Vijana waliopita JKT hadi mwaka 2014 ni 104,594. Kati ya hao, 34,291 waliingia kwa mpango wa kujitolea ambapo asilimia 70 waliajiriwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Asilimia 30 inayobaki, sawa na vijana 2,000, wanarudi nyumbani kila mwaka.
Previous
Next Post »