WAATHIRIKA WA MAFURIKO WAANZA KUZIHAMA NYUMBA ZAO. - Rhevan Media

WAATHIRIKA WA MAFURIKO WAANZA KUZIHAMA NYUMBA ZAO.

Waaathirika wa mvua za masika waliopo kata za Magaoni na Usagara jijini Tanga ambao wamezihama nyumba zao kwa sababu ya kujaa maji kulikosababishwa na kukosekana kwa mifereji ya kupeleka maji hayo baharini, wamewalalamikia viongozi wa halmashauri ya jiji la Tanga kwa kushirikiana na madiwani kuachana na migogoro ya kisiasa na badala yake waelekeze nguvu zao katika zoezi la kunusuru maisha ya wananchi walioathika na mvua za mafuriko.
Wakizungumza na ITV katika maeneo yaliyoathirika na tatizo hilo waathirika hao wamesema hali ya usalama wa afya zao upo hatarini kwa sababu kujaa maji ndani ya nyumba zao ambayo mengine ni machafu baada ya vyoo kufurika kutokana na mvua za mafuriko kumewapa hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya milipuko.
 
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Magaoni Bwana Ramadhani Malodi ameiomba halmashauri kuwapelekea gari la kupasua mfereji ambalo litasaidia kuondoa maji hayo kwa sababu katika eneo lake kaya zaidi ya 75 zimehama nyumba zao huku baadhi yao wakikosa hata mahali pa kujihifadhi.
 
Kufuatia hatua hiyo baadhi ya madiwani wa halmashauri ya jiji la Tanga wamewatupia lawama viongozi wa halmashauri na serikali kwa ujumla kwa kushindwa kujali adha hiyo ambayo imesababisha hata baadhi ya watu kupoteza maisha kwa sababu ya mvua za masika hivyo wameshauri shule za msingi zifungwe ili waathirika waweze kupata makazi ya muda huku suala la uchimbaji wa mifereji likiendelea kushughulikiwa.
Previous
Next Post »