NJOMBE ,IRINGA ,MBEYA NI HATARI KWA AFYA YAKABILIA NA MAAMBUKIZI MAKUBWA. - Rhevan Media

NJOMBE ,IRINGA ,MBEYA NI HATARI KWA AFYA YAKABILIA NA MAAMBUKIZI MAKUBWA.

MIKOA ya Njombe, Iringa na Mbeya imetajwa kuwa na maambukizi makubwa zaidi ya virusi vya Ukimwi (VVU) nchini kutokana na mwingiliano watu unaosababishwa na shughuli za kiuchumi.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Tume ya kudhibiti Ukimwi (Tacaids) Mkoa wa Mbeya, Edwin Mweleka, wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye utambulisho wa mradi wa ushirikishaji wa wananchi wanaoishi na virusi vya Ukimwi wa ‘Sauti yetu’ unaofadhiliwa na wananchi wa Marekani kuipitia Shirika la USAID.
Mweleka alisema Mkoa wa Njombe unaongoza kwa kuwa na asilimia 14.8, ukifuatiwa na Iringa wenye asilimia 9.1 na Mbeya unashika nafasi ya tatu ukiwa na asilimia tisa.
Alisema mradi huo wa ‘Sauti Yetu’ utasaidia kupunguza maambukizi hayo.
“Tunashukuru wenzetu wa Marekani kwa kutusaidia kufadhili mradi huu wa Sauti yetu kupitia shirika la USAID, na naamini kwa mikoa yetu hii yenye maambukizi makubwa, mradi huu utakuwa msaada mkubwa katika kupunguza maambukizi,” alisema.
“Mikoa ya ukanda wetu wa Nyanda za Juu Kusini ndiyo inayooongoza kwa maambukizi ikiongozwa na Njombe ambao ndio mkoa unao ongoza kitaifa wenye asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa wenye asilimia 9.1 huku Mbeya tukishika nafasi ya tatu kwa asilimia tisa, hivyo kampeni itakayokuwa inaendeshwa kupitia ‘Sauti yetu’ tunatarajia itusaidie kupunguza maambukizi hayo mpaka kufikia sifuri tatu,” alisisitiza.
Mweleka alisema kuwa mikoa ya Mbeya na Iringa haijawahi kutoka kwenye orodha ya mikoa mitatu yenye maambukizi makubwa tangu tafiti zilipoanza kufanyika katika miaka ya 2003/2004.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini, Justine Mwinuka, alisema mradi huo unatekelezwa katika halmashauri 46 zilizopewa kipaumbele nchi nzima huku katika Mkoa wa Mbeya zikihusika halmashauri tatu ambazo ni Mbeya jiji, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Alisema kuwa watu wanaolengwa kwenye mradi huo ni wale wanaoishi na VVU pamoja na wenye kifua kikuu kwa madai kuwa magonjwa hayo yana uhusiano wa moja kwa moja.
Alisema kuwa mradi huu unatambulishwa kwa waratibu wa Ukimwi shughuli za Ukimwi ngazi ya halmashauri pamoja na watendaji wa mabaraza ya watu wanaoishi na VVU ngazi za wilaya (Konga)
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo wa ‘Sauti Yetu’, Rachel Jacob, alisema changamoto inayowakumba watu wanaoishi na VVU kwa sasa ni unyanyapaa binafsi hali ambayo huwafanya watu hao kuishi kwa wasiwasi wakati wote.
Alisema lengo kubwa la mradi huo ni kutoa hamasa kwa jamii kupima afya zao kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa ili kila mtu aweze kuijua afya yake na wale wanaokutwa na maambukizi waweze kuanzishiwa dawa.
Jacob alisema kuwa Mradi huo ulianza kutekelezwa tangu mwezi Oktoba 2015 na utakamilika mwezi Oktoba mwaka 2019.
Previous
Next Post »