Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuwapongeza wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge ulioambatana na kutambulisha magari ya kubebea wanafunzi katika uwanja wa Mashujaa, mjini hapa, alisema amepitia mpango wa shirika hilo na kujiridhisha kuwa mikoa hiyo haimo katika mradi huo.
Alisema mpango wa mwaka 2016/2017 wa TPDC unaonyesha mkakati wao wa kuongeza megawati za umeme ambazo zitatumika Tanzania nzima kupitia mradi wa bomba la gesi linalotoka Madimba mpaka Kinyerezi, Dar es Salaam, lakini katika mpango wa pili ambao ni wa kusambaza gesi nyumbani, mikoa hiyo haimo.
“Cha ajabu katika mpango wa serikali ndugu zangu pamoja na kwamba huu mkakati na utekelezaji unaanza katika bajeti ijayo, kusambaza mabomba ya gesi nyumbani, Mtwara na Lindi ambako gesi inatoka haipo ndugu zangu.
Mtwara na Lindi inakotoka gesi kwenye ule mpango haijawekwa kwamba wana Mtwara na sisi tuweze kutumia gesi kwa ajili ya kupikia na mambo mengine tuepukane na kuni, haijawekwa. Ni mambo ya kusikitisha kwa kweli..” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mbunge inapingana na maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio, ambayo alimweleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipofanya ziara katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba, Februari 27, mwaka huu.
“Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa na TPDC ni pamoja na mradi wa uagizaji wa mafuta ya hifadhi ya taifa, mradi wa usambazaji gesi majumbani (nyumbani) katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam,” alisema Dk. Mataragio katika taarifa yake.
Mbali na maelezo hayo, Meneja Biashara ya Gesi wa TPDC, Emmanuel Gilbert, aliwahi kuwaeleza waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa semina ya siku moja kwa waandishi ya kuwajengea uwezo wa masuala ya mafuta na gesi, kuwa shirika liko katika mchakato wa ujenzi wa mradi huo na kwamba upembuzi ya kinifu katika mikoa ya Lindi na Mtwara umekamilika.
Alisema mradi huo ambao utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi kwa sasa zinasubiriwa fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kuanza usanifu wa michoro katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu hiyo.
Kwa mujibu wa Gilbert, mtandao wa kutandaza mabomba ya mradi huo utakuwa na urefu wa kilomita 17 kwa mkoa wa Mtwara na unatarajiwa kuunganisha nyumba 11,000 na magari 4,000 ambayo yatakuwa na uwezo wa kuamua kutumia nishati ya gesi au mafuta na kilomita 11 kwa mkoa wa Lindi.
Sign up here with your email