Mashindano ya kitaifa ya vilabu ya mchezo wa judo yanatarajiwa kuanza Mei 28 mwaka huu visiwani Zanzibar kwa kushirikisha vilabu mbalimbali vya Tanzania Bara na Visiwani.
Kocha wa Timu ya Taifa ya Judo Zaidi Khamis amesema, kila klabu inataarifa juu ya mashindano hayo na anaamini vilabu hivyo vitaitikia wito wa kushiriki mashindano hayo ambayo ni makubwa kwa kila mchezaji kuonyesha kiwango chake.
Zaidi amesema, mashindano hayo yanasaidia kuweza kupata vijana ambao wataweza kuunda timu ya Taifa ya Judo ambayo itashiriki mashindano mbalimbali yaliyo katika kalenda ya Shirikisho.
Amesema, hawajafanya mashindano ya Judo kwa muda mrefu hivyo mashindano hayo yatasaidia kuwaweka vizuri wachezaji japo hawana uwezo wa kupeleka timu nje ya nchi lakini wataangalia ni mashindano gani ambayo wataweza kushiriki.
Zaid amesema, kwa hivi sasa timu nyingi zinaangalia zaidi mashindano ya Olimpiki na wao kama chama pia waliomba nafasi maalumu ya kupeleka timu katika mashindano ya Olimpiki Rio nchini Brazili na wanaamini mashindano ya vilabu yatawasaidia kuwajenga kwa ajili ya mashindano hayo endapo watapata nafasi.
Sign up here with your email
