MADIWANI 34 WA UKAWA WAMTIKISA MKUU WA MKOA WA MBEYA. - Rhevan Media

MADIWANI 34 WA UKAWA WAMTIKISA MKUU WA MKOA WA MBEYA.





Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34 kususia kikao chake cha kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji hilo.

Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda mfupi kabla ya Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi, wazee maarufu, viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote kwa niaba ya madiwani wake.

Hata hivyo, Meya Mwashilindi alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”

Baada ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya, kisha akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema na kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa ambazo tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi kupuuzwa kwa kiasi hiki.”

Previous
Next Post »