Ripoti ya waangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015, imeshauri kuangaliwa upya kwa sheria za uchaguzi ikiwa ni pamoja na mifumo ya uhesabuji wa kura katika ngazi zote hasa nafasi ya Urais.
Ripoti hiyo yenye kurasa zaidi ya 300, iliyozinduliwa Dar es Salaam imeonyesha pia elimu ndogo ya mpiga kura ambapo zaidi ya asilimia 3.29 ya kura za Urais ziliharibika ukilinganisha na asilimia 2.6 ya kura za Urais zilizoharibika kwa mwaka 2010, ambapo pia imeipongeza tume ya uchaguzi kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Aidha ripoti hiyo imesema licha ya tukio la Oktoba 29 mwaka 2015 la kunyanganywa kwa komputa za waangalizi wa uchaguzi wa kituo cha LHRC, uchaguzi wa mwaka 2015, haukuwa na vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ukilinganisha na mwaka 2010, ambapo pia imeshauri kuwa ni wakati muafaka kwa uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na tume ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Fransis Mutungi pamoja na masuala mengine amesema kupitia ripoti kama hizo zinaifanya serikali kuona namna bora zaidi ya kuzidi kuandaa chaguzi huru na haki.
Wawakilishi wa vyama vya siasa waliohudhuliwa uzinduzi wa ripoti hiyo wamepongeza mapendekezo ya ripoti hiyo kwa serikali ambayo ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa Katiba mpya, uundwaji wa tume huru ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa mgombea binafsi, huku vyama vilivyotajwa na ripoti kuwa ni vidogo vikiikosoa kauli hiyo.Kwa mujibu wa TACCEO,inasema uchaguzi wa mwaka 2015, ulikuwa na waangalizi wa ndani zaidi ya 10,000 huku sheria za gharama ya uchaguzi zikitakiwa kuangaliwa kwa usawa wa vyama kwani kumeonekana sheria hiyo kuwa msumemo kwa baadhi ya vyama pekee.
Sign up here with your email