BWAWA LA KIDATU LAJAA LATISHIA USALAMA WA WANANCHI. - Rhevan Media

BWAWA LA KIDATU LAJAA LATISHIA USALAMA WA WANANCHI.


Mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha kuongezeka kwa maji katika bwawa la Kidatu, hivyo kuvuka kiwango chake cha kawaida.

Ujazo unaotakiwa katika bwawa hilo ni mita 450 kutoka usawa wa bahari, lakini hadi jana ulifikia mita 450.5, jambo linalohatarisha kuharibika kwa miundombinu na maji kuwaathiri wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi, kilimo na kuishi kando ya Mto Ruaha Mkuu.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, wametembelea maeneo hayo na kuamuru kufunguliwa kwa mageti makubwa yaliyojengwa maalum kuzuia maji, ambayo kwa sasa yanapita juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchecim Mramba, alisema kuharibika kwa bwawa hilo iwapo maji hayo yatashindwa kudhibitiwa, mbali na kuathiri wananchi, kutasababisha hasara kubwa kwa kituo hicho cha kuzalisha umeme.
“Tunasema hii ni neema, kwa vile mwaka jana tulikuja hapa na maji kwenye bwawa yalikuwa chini ya kiwango, mita 433 kutoka usawa wa bahari.
Lakini mwaka huu maji yamekuwa mengi na ya kutosha. Hali kama hii iliwahi kutokea mwaka 2007 na tulilazimika kufungua mageti kwa dharura ili kupunguza maji. Inabidi kupunguza maji ili kuhakikisha bwawa na miundombinu yake inabaki salama,” alisema.
Alisema iwapo maji yataachwa kuendelea kupita juu ya mageti na yakaharibu miundombinu, maafa yanayoweza kujitokeza ni makubwa na ambayo hayajawahi kuripotiwa nchini.
Kwa mujibu wa Mramba, wingi huo wa maji unatokana na maji ya mvua zinazonyesha mkoa wa Morogoro yakipitia katika Mto Lukosi na Iyovi, inayopeleka maji Mto Ruaha Mkuu na kwamba walilazimika kuzuia maji zaidi waliyokuwa wakipokea kutoka bwawa la Mtera.
“Bwawa la Mtera kwa sasa nalo limejaa maji, lakini si kwa zaidi ya kiwango. Mtera ina uwezo wa kuchukua maji mita za ujazo 697.14 kutoka usawa wa bahari na sasa yamefikia mita 698.3. bado kama asilimia 1.4, likijaa nalo tutalazimika kufungua,” alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Dk. Stephen Kebwe, alisema wameruhusu Tanesco kupunguza kiasi cha maji kilichoongezeka katika bwawa hilo, huku akitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari hasa wakati huu mvua zinapoendelea kunyesha ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Previous
Next Post »