AMNESTY INTERNATIONL YATAKA KUFANYIKE UCHUNGUZI WA MAUAJI YA WAISLAMU NIGERIA. - Rhevan Media

AMNESTY INTERNATIONL YATAKA KUFANYIKE UCHUNGUZI WA MAUAJI YA WAISLAMU NIGERIA.


Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mauaji ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria.

Taasisi hiyo ya kimataifa imesisitiza kuwa, matamshi yaliyotolewa na afisa mmoja wa serikali ya Nigeria aliyesema kuwa maiti 347 za wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini humo zimezikwa kwa siri katika kaburi la umati, yanapaswa kuchunguzwa na wahusika wa uhalifu huo wachukuliwe hatua.

Afisa huyo wa serikli ya Nigeria amewaambi wachunguzi kuhusu tukio chungu la kuuawa mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika jimbo la Kaduna kwamba, maiti hizo kwanza ziliwekwa katika ghala la jeshi la nchi hiyo na baadaye zilizikwa katika kuburi la umati.

Wataalamu wa Amnesty International wanasema, kaburi hilo la umati linapaswa kulindwa baada ya maiti zilizomo kufanyiwa uchunguzi kamili wa kisheria.

Disemba mwaka jana jeshi la Nigeria lilishambulia makazi ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky na kituo cha kidini cha Waislamu wa mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna na kuua mamia miongoni mwao. Sheikh Zakzaky na wanachama wengine wa Harakati ya Kiislamu pia walitiwa nguvuni na hadi sasa bado wanashikiliwa na jeshi la Nigeria.

Mustafa Muhammad ambaye ni mwanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema, hali ya kiafya ya kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky, si nzuri na kwamba baadhi ya wanachama wa harakati hiyo walimtembelea kiongozi huyo wiki iliyopita.

Habari za kufichuliwa kaburi la umati la Waislamu waliouawa na jeshi nchini Nigeria imezusha tena mjadala mkubwa katika duru mbalimbali kuhusu hali ya Waislamu wa nchi hiyo.

Bwana Mustafa Muhammad anasema katika uwanja huo kwamba, hali ya Waislamu wa Nigeria si nzuri na kwamba serikali imezidisha ukandamizaji dhidi ya taasisi na jumuiya za kidini.

Mwanachama huyo mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema, kupanuka zaidi kwa dini ya Uislamu sahihi chini ya mafundisho ya Ahlul Bait na Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume Muhammad (saw) katika baadhi ya nchi za maghaibi mwa Afrika kama Nigeria, Cameroon, Niger na Ghana kunawakasirisha baadhi ya maafisa wa serikali na madola ya kigeni ambayo yanatumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kuwakandamiza Waislamu wasio na hatia yoyote.

Habari ya kufichuliwa kaburi la umati lenye miili ya Waislamu 347 wafuasi wa Harakati ya Kiislamu huko Zaria imetilia mkazo udharura wa kufanyika uchunguzi kuhusu mauaji yaliyofanywa na jeshi al Nigeria dhidi ya Waislamu hao.


Ingwa serikali ya Nigeria bado haijasema lolote kuhusu habari hiyo lakini inatupasa kusubiri na kuona jamii ya kimataifa hususan nchi zinazodai kuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu, zitachukua hatua gani katika uwanja huo.
Previous
Next Post »