AMCOS KUIPELEKA SERIKALI YA MBEYA MAHAKAMANI. - Rhevan Media

AMCOS KUIPELEKA SERIKALI YA MBEYA MAHAKAMANI.

CHAMA cha Ushirika cha Luhanga Amcos, jijini Mbeya kina mpango wa kuipeleka Serikali ya Mkoa wa Mbeya mahakamani kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, kutangaza kulirudisha shamba lililokuwa linamilikiwa na chama hicho kwa wananchi.

Wakizungumza mbele ya vyombo vya habari mkoani hapa, viongozi na wanachama wa chama hicho walisema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, alitangaza kurudisha shamba lao ambalo wanalimiliki kihalali lenye ukubwa wa hekta 5000 kwa wananchi wa Kijiji cha Luhanga, wilayani Mbarali bila kuwashirikisha, hali inayoweza kusababisha mgogoro wa ardhi.
Mwenyekiti wa chama hicho, Merkion Bagule, alisema baada ya uamuzi huo wa Mkuu wa Mkoa, Bodi ya Luhanga Amcos, iliamua kufungua kesi mahakamani ili kunusuru shamba lao, lakini wakaona ni busara waitishe mkutano mkuu kwa dharura ili kupata baraka za chama.
Alisema lengo lao ni kutaka mahakama iweke zuio la shamba lao kutofanyiwa kitu chochote wakati wanapotarajia kufungua kesi ya msingi.
Alisema mkutano mkuu huo ulikuwa ni wa kutoa baraka za chama kwenda jijini Dar es Salaam ili kumuona Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi na kwamba ikiwezekana watamuona hata Rais.
“Sisi tuliposikia kwenye vyombo vya habari kuwa Mkuu wa mkoa amerudisha shamba letu ambalo tunalimiliki kihalali kwa wananchi, tuliamua kuitisha kikao cha bodi ambacho kiliamua kuwa tufungue kesi dhidi ya serikali ili kupinga uamuzi huo wa mkuu wa mkoa,” alisema na kuongeza.
“Lakini tuliona sio busara kufanya uamuzi wenyewe ndio maana tumeitisha mkutano mkuu kwa dharura ili tuweze kupata baraka za wanachama, na mkutano huu unatakiwa kutoa baraka za Kufungua kesi pamoja na kwenda kumuona Waziri mwenye dhamana ya ardhi na Rais ili kilio chetu kiweze kusikilizwa,” alisema.
Naye Katibu wa chama hicho, Jimmy Mwaikenda, alisema chama kina nyaraka zote zinazoonyesha umiliki wa shamba hilo na kwamba mkuu wa mkoa amefanya uamuzi wa kukurupuka ambao una lengo la kudidimiza haki.
Alisema kuwa chanzo cha mgogoro wa shamba hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulamhussen Kifu, ambaye anadaiwa kuwa tangu alipohamishiwa wilayani Mbarali amekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya chama hicho.
Aliongeza kuwa wakuu wote wa wilaya hiyo waliotangulia walikuwa wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa chama hicho na walikuwa wametoa nyaraka za umiliki wake ndio maana walikuwa wanasaidia katika shughuli za maendeleo.
“Mkuu wa Wilaya ya Mbarali ndio tatizo maana tangu tumeanza tulikuwa tunapata ushirikiano kutoka kwa wakuu wote wa wilaya hiyo, ndio maana tumekuwa tukisaidia shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa ofisi ya kijiji, pamoja na huduma za maji, lakini alipoingia huyu bwana ndipo matatizo yalianzia,” alisema Mwaikenda.
Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa chama hicho, walishauri wakati uongozi wa chama unaendelea na harakati hizo kuna sababu pia kwenda kuongea na wananchi wa Luhanga ili watoe maoni yao.
Katika mkutano huo chama hicho kiliunda kamati yenye wajumbe 11 ambao ndio watakuwa wanashughulikia mambo yote kuanzia kufungua kesi mpaka kwenda kumuona Rais.
Previous
Next Post »