Waziri wa Maji, Gerson Lwenge awasimamisha kazi mameneja 9 wa DAWASCO, mwingine atakayechukuliwa hatua ni Mkurugenzi aliyestaafu Wanatuhumiwa kulisababishia shirika hilo hasara ya Shilingi bilioni 2.8 Awali utumbuaji majipu, ambao unalenga kuondoa ufisadi na uzembe katika utumishi wa umma, ulikuwa ukihusisha watendaji walio kazini, lakini jana Waziri Lwenge alisema aliyehusika kwenye tuhuma hizo za ufisadi wa kitaasisi atachukuliwa hatua hata kama ameshaachia nafasi yake. Akizungumza katika mkutano wake na watendaji wakuu wa shirika hilo, Waziri Lwenge alisema kusimamishwa kwa watumishi hao ni kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika njama za kuiunganisha maji kampuni ya Strabag bila kufuata utaratibu. Aliwataja watumishi waliosimamishwa kuwa ni Peter Chacha, Regnald Kessy, Theresia Mlengu, Josper Kilango, Fred Mapunda, Mvano Mandawa, Emanuel Gulupa, Raymond Kapyela na Jumanne Mapunda. Waziri Lwenge pia ameagiza aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo ambaye alistaafu, Jakson Midala naye achunguzwe ushiriki wake katika njama hizo kwa kuwa zilifanyika wakati wa uongozi wake. Sambamba na maagizo hayo, waziri huyo wa maji ametoa siku 14 kwa Strabag kulipa kiasi hicho cha pesa kilichokwepwa vinginevyo hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo. Strabag ni kampunii ya ujenzi inayoshughulikia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT). Waziri alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu wa shirika hilo la maji walifanikisha kuunganisha maji bila kupata vibali na kufuata utaratibu.
Sign up here with your email