
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema kuwa, uingiliaji wa kigeni ndio chanzo kikuu cha kuibuka mgogoro na tofauti kuhusiana na kadhia ya mrithi wake.
Rais Mugabe ameyasema hayo mbele ya mawaziri, wanadiplomasia wa kigeni na wawakilishi wa vyama tawala vya Angola, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania na Botswana.
Aidha amesisitiza kuwa, kama ilivyokuwa katika kipindi cha ukoloni barani Afrika, Uingereza na Marekani zimekuwa zikitumia hila za kutoa fedha na mali kwa wajumbe wa chama tawala nchini humo, ili kuibua tofauti ndani ya chama hicho.
Rais huyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980, amejiepusha kumtangaza mtu ambaye atachukua nafasi ya uongozi baada yake.
Pamoja na hali hiyo, duru za kisiasa zimekuwa zikimtaja Emmerson Mnangagwa, ambaye ni makamu wake wa sasa kuwa chaguo bora la kumrithi Rais Mugabe.
Hata hivyo Bi. Grace Mugabe, mke wa rais huyo anaonekana kuwa mshindani mkuu wa Mnangagwa. Emmerson Mnangagwa ni mwanasiasa mkongwe nchini Zimbabwe ambaye tangu nchi hiyo ijipatie uhuru, amekuwa na nyadhifa mbalimbali katika Baraza la Mawaziri katika serikali ya Rais Mugabe.
Hadi kufikia mwaka 2000 shakhsia huyo alikuwa akihudumu kama waziri nchini humo. Miaka mitano baadaye alikuwa spika wa bunge huku akiongoza pia Wizara ya Sheria, kabla ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais baada ya kuondolewa katika nafasi hiyo Joice Moyo hapo mwezi Disemba mwaka 2014.
Aidha Mnangagwa ambaye alikuwa mshirika wa Rais Mugabe katika kupigania uhuru wa nchi hiyo, kwa muda aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha ZANU–PF.
Kwa kuzingatia hali hiyo, harakati za siri za mwanasiasa huyo kwa ajili ya kuvutia uungaji mkono wa viongozi wa chama tawala na jeshi la nchi hiyo, zinabainisha azma yake ya kutaka kuwania nafasi ya urais wa taifa hilo. Ushindani baina ya Emmerson Mnangagwa na Bi. Grace Mugabe kwa ajili ya kuwania nafasi ya urithi baada ya Rais Mugabe, ulishika kasi tarehe 15 mwezi Juni mwaka 2014.
Katika kipindi hicho mke huyo wa Rais Mugabe alidai kuwa, baadhi ya maafisa wa ngazi za juu jeshini kwa kushirikiana na Mnangagwa, walikuwa wanapanga kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali ya mumewe.
Kufuatia madai ya jaribio hilo lililofeli la mapinduzi ya kijeshi, jumla ya askari 400 walitiwa mbaroni.
Kwa mujibu wa Bi. Grace Mugabe, wafanyamapinduzi walikuwa wamepanga kumuua Rais Mugabe na kwa kushirikiana na baadhi ya majenerali wa jeshi, waweze kuasisi utawala wa kijeshi nchini Zimbabwe, ingawa madai hayo hayakuthibitishwa.
Hivi sasa duru za habari zinaelezea kuwepo harakati mpya za kisiasa kwa ajili ya kumuengua Bwana Emmerson Mnangagwa kutoka chama tawala ZANU-PF. Tarehe 25 mwezi huu, magazeti ya mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe yaliandika kuwepo mpango wa kumsaili mwanasiasa huyo katika jimbo la Mashonaland, magharibi mwa nchi.
Kabla ya hapo pia Grace Mugabe alidai kuwa, baadhi ya viongozi wa chama tawala na askari jeshini, walikuwa wamekusudia kumuua mtoto wake.
Kwa mujibu wa magazeti ya nchi hiyo, aliyekuwa analengwa katika tuhuma hizo alikuwa ni Mnangagwa mwenyewe.
Pamoja na hali hiyo, tuhuma mtawalia dhidi ya shakhsia huyo, bado hazijaweza kupunguza nafasi yake ya kisiasa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Hivi sasa hatua ya Rais Robert Mugabe ya kuzungumzia uingiliaji wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya Zimbabwe, bila kujali ukweli au uongo wake, yanabainisha kuwepo mjadala na tofauti kubwa kuhusu nani atakuwa mrithi wake chamani.
Sign up here with your email
