DUKUDUKU LA WATANZANIA ELIMU BURE. - Rhevan Media

DUKUDUKU LA WATANZANIA ELIMU BURE.


Twaweza: Dukuduku za wananchi kuhusu mpango wa elimu bure nchini zifanyiwe kazi na serikali Shirika la Kitafiti la Twaweza, limezindua taarifa ya utafiti katika sekta ya elimu Tanzania, na kubainisha kuwa wananchi wanaamini kwamba, asilimia 88 ya wananchi wanaamini kuwa ahadi ya elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa; kwamba, asilimia 76 wanaamini kuwa elimu bure itakuwa elimu bora zaidi; na kwamba, asilimia 15 wanaamini kuwa mpango wa elimu ya bure hautaboresha maarifa ya wanafunzi kutokana na ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wanafunzi ambao utatumia rasilimali nyingi. Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la “Mwanga Mpya? Maoni ya Wananchi Kuhusu Mabadiliko Kwenye Sekta ya Elimu.” Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wenye uwakilishi kutoka kada na kona zote kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Takwimu zilizokusanywa kati ya tarehe 10 Desemba, 2015 na tarehe 2 Januari 2016, kutoka kwa watu 1,894 waliohojiwa Tanzania Bara. Utafiti huu, pia unaonyesha kwamba, mpango wa utoaji wa elimu bila malipo pamoja na kukomesha michango shuleni umekuja katika wakati ambapo wazazi wengi walikuwa wanaelemewa na michango ya shule. Kwa ujumla, asilimia 89 ya wazazi wanakiri kulipa michango shuleni; asilimia 80 wakiripoti kulipa mpaka TZS 50,000 kwa mwaka, huku asilimia 8 wakilipa zaidi ya TZS 100,000 kwa mwaka. Asilimia 49 wanaamini kwamba michango yao haitumiki ipasavyo na asilimia 58 wanasema michango hiyo haijaidhinishwa na serikali. Asilimia 89 wanasema walimu hutumia michango hii kujiongezea kipato. Kwa mujibu wa wazazi, michango hutumika kulipia ulinzi (asilimia 66), majaribio (asilimia 57) na madawati (asilimia 34), huku kiwango kidogo kikielekezwa kwenye mahafali (asilimia 4), pamoja na safari za kishule (asilimia 4).
Previous
Next Post »