Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Ulinzi na Usalama ya Mtaa wa Mbagala-Kiburugwa, Bw.Kassim Mohammed Mnyoge, akizungumzia maagizo hayo |
………………………………………………………………………………………………………………..
NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
WAKAZI wa Mtaa wa Mbagala- Kiburugwa, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, wamefanya kikao Jumapili Novemba
20, 2016, cha kujadili maagizo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP), Gilles Muroto kuhusu
masuala ya Ulinzi na Usalama ngazi ya Mtaa.
Akizungumza kwenye kikao hicho,
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata Bw.Saleh Kaitani, alisema, kikao hicho
kitajadili mambo mawili, mosi ni maagizo ya SACP Muroto na pili ni
masuala ya mpango wa kusaidia kaya masikini wa TASAF.
Kusuhusu suala la ulinzi na
usalama, Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Ulinzi na Usalama ya Mtaa huo,
Bw.Kassim Mohammed Mnyoge alisema, SACP Muroto katika kikao chake na
watendaji kilichofanyika Oktoba 28, 2016 kwenye shule ya msingi Kigungi,
alitoa maagizo kadhaa kuhusu hatua za kuchukua katika kuhakikisha
wananchi wanashirikishwa katika suala la ulinzi na usala.
“Kila mjumbe wa mtaa kwa
kushirikiana na Mratibu, waorodheshe katika daftari wakazi wa mtaa
husika ili kujua idadi yao na shughuli wanazofanya.” Alisema Bw. Kassim
wakati akiwasilisha taarifa kwa wananchi.
Mtaa wa Kiburugwa una wakazi wanaofikia 18,000 kwa mujibu wa Bw. Kassim.
Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo la Ulinzi na Usalama, Bw. Kassim alisema, SACP Muroto
ameagiza wananchi mjadili jinsi ya kushiriki katuika suala la ulinzi na usalama kwenye mitaa.
Kila mwenye nyumba, anapotembelewa na mgeni ni lazima akatoe taarifa kwa mjumbe wa nyumba kumi
au kwa mratibu wa eneo husika, lakini pia kila mwananchi lazima
ashiriki kwenye suala la ulizni na akikaidi Mjumbe wa mtaa apelike
taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa ili taarifa hiyo imfikia RPC
kwa hatua za kisheria ambazo
adhabu zake ni faini ya shilingi elfu 50,000 au kifungo cha miezi sita jela au vyote kwa pamoja.
Maagizo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja wazazi kuwadhibiti watoto wao, na endapo mtoto mwenye umri
chini ya miaka 18 atajihusisha na vitendo vya kihalifu kama kujiunga
na makundi ya “panya road”, basi mzazi wa mtoto huyo atakamatwa kwa vile
ni jukumu lake kuhakikisha mtoto huyo anakuwa katika maadili mema.
Wakichangia kwenye mjadala huo, wananchi wengi wamekubaliana na maagizo hayo ya kushiriki
kwenye ulinzi lakini wakaonyesha wasiwasi namna ya utekelezaji wake.
“Ninapenda nijulishwe, ulinzi huu
ambao wananchi tunatakiwa kushiriki ni wa namna gani, maana hali ya
sasa sio kama ile ya zamani ya enzi za Mrema, mambo ya sungusungu
kutembea na panga nataka kujua tunalindaje na usalama wetu ukoje endapo
nitadhurika.” Aliuliza mwananchi mmoja Bw.Hamisi Omary Libinongi.
Mwananchi mwingine, alisema, ni
vema wananchi wanapolinda wakaongozana na askari wenye silaha, kwani
wahalifu wa sasa, wanabeba silaha nzito nzito na kwamba itakuwa hatari
kwa mwananchi kufanya doria kwa kutumia panga pekee.
Akijibu hoja kuhusu jinsi ya
ushiriki wa wananchi katika ulinzi, Mwneyekiti wa Serikali ya Mtaa huo,
Bw.Said Mwinshehe Ng’agi, alisema, wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi
katika suala hilo la ulinzi, kwani kila kundi la wananchi wanaolinda
kwenye eneo fulani, wataongozana na askari wawili wenye silaha.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata
hiyo ya Kiburugwa, Bw.Salehe Kaitani, amesema maagizo hayo ni ya
serikali na wananchi hawana buni kushirikiana ili kuyatekeleza.
“Wananchi tunapaswa kutekeleza maagizo haya ya Jeshi la polisi, najua
zipo changamoto za baadhi ya askari kutokuwa waaminifu, lakini kama
mjuavyo askari wa namna hii
ambao hawana wito, wamekuwa wakichukuliwa hatua na nyinyi
wananchi toeni taarifa kwa viongozi kama mnakutana na askari wanaodai
rushwa.” Alisema Bw. Laitani.
Sign up here with your email